Watu wawili wanaoshukiwa kuwa walanguzi wa dawa za kulevya walikamatwa leo katika msako uliotekelezwa na maafisa wa mamlaka ya kukabiliana na matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya – NACADA.
Msako huo uliotekelezwa katika kijiji cha Kabaa, eneo la Mbiuni kaunti ya Makueni ulifuatia taarifa walizopokea maafisa kutoka kwa umma na ni sehemu ya msako mkubwa dhidi ya dawa za kulevya kote nchini.
Chini ya uongozi wa Nicholas Kosgei ambaye ni mkuu mwandamizi wa polisi, maafisa hao walipata mafungu 20 na misokoto 87 ya bhangi pamoja na vifaa kama makaratasi ya kuunda misokoto, makasi na pesa taslimu zinazoaminika kutokana na mauzo ya bhangi.
Washukiwa hao walifikishwa mahakamani kwa makosa ya kulangua dawa za kulevya.
Afisa mkuu mtendaji wa NACADA Anthony Omerikwa alisifia maafisa waliohusika katika msako huo na wakenya waliowapasha habari zilizosababisha kukamatwa kwa wawili hao.
“Kukamatwa kwa wawili hawa ni ujumbe kwa walanguzi wa dawa za kulevya na wanaouza kwa siku zao zimewadia.” alisema Omerikwa huku akisisitiza kwamba hawatalegeza kamba katika msako unaolenga kuharibu kabisa mtandao wa dawa za kulevya nchini.
“Hata eneo lako liwe mbali namna gani, iwapo unahusika na ulanguzi wa dawa za kulevya tutakupata.” alionya Afisa huyo mkuu mtendaji wa NACADA.
Omerikwa alihimiza wakenya pia waendelee kushirikiana na maafisa wa NACADA kwa kutoa habari kupitia nambari ya simu ambayo ni 1192. Kulingana naye, kuhusisha jamii ni muhimu katika juhudi za kumaliza dawa za kulevya nchini.
NACADA imethibitisha kwamba oparesheni sawia zitaendelezwa katia muda wa wiki kadhaa zijazo na zinalenga wasambazaji wa dawa za kulevya.