NACADA yaimarisha vita dhidi ya utumizi wa Shisha

Tom Mathinji
1 Min Read
NACADA yaimarisha vita dhidi ya Shisha.

Halmashauri ya kukabiliana na utumizi wa mihadarati NACADA,imeendeleza operesheni yake dhidi ya utumizi wa Shisha, huku washukiwa wawili wakinaswa kaunti ya Laikipia kwa kuendesha biashara ya uuzaji bidhaa hiyo iliyoharamishwa hapa nchini.

Katika operesheni hiyo iliyoongozwa na afisa mkuu wa polisi Nicholas Kosgey, halmashauri hiyo ililenga maeneo kadhaa ya burudani yaliyoshukiwa kukiuka marufuku dhidi ya shisha, ambapo wawili hao walipatikana wakiuza shisha na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Nanyuki wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa, alitoa onyo kali kwa wle ambao bado wanatekeleza biashara haramu ya shisha, kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Uuzaji na utumizi wa shisha ni haramu hapa nchini, na NACADA haitalegeza kamba katika juhudi zake za kutokomeza utumizi huo ambao ni hatari kwa afya ya umma,” alisema Omerikwa.

NACADA imezidisha msako wa biashara na utumizi wa shisha kote nchini, hususan katika sehemu za burudani kuhakikisha marufuku dhidi ya shisha ya mwaka 2017 inatekelezwa kikamilifu.

Wito umetolewa kwa umma kuunga mkono juhudi za NACADA za kukabiliana na uuzaji na utumizi wa shisha, kwa kuripoti wanaoshiriki shughuli hiyo.

“Halmashauri hii imejitolea kuwalinda vijana na umma kwa jumla dhidi ya hatari za utumizi wa mihadarati,” aliongeza Omerikwa.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article