Mwigizaji na mchekeshaji wa Canada na Marekani Jim Carrey amejipata akiangaziwa sana kwenye mitandao ya kijamii kisa na maana mwonekano wake mpya.
Msanii huyo wa umri wa miaka 64 sasa, alihudhuria awamu ya 51 ya tuzo za César jijini Paris Alhamisi iliyopita ambapo alionekana tofauti na jinsi mashabiki walivyomfahamu awali.
Carrey alialikwa kwa hafla hiyo kupokea tuzo ya heshima ya César, tuzo zinazochukuliwa kuwa za hadhi ya juu zaidi nchini Ufaransa katika tasnia ya filamu.
Alikuwa amevaa suti ya rangi nyeusi na aliamua kutozungumza na wanahabari katika eneo la zulia jekundu.
Uso wake awali ulikuwa unaonekana kama wa mtu aliyekula chumvi na sasa unaonekana kujaa vizuri na unaonekana pia kama wa mtu wa umri mdogo kuliko miaka yake 64.
Carrey sasa anajiunga na waigizaji wengine waliopokea tuzo hiyo ya heshima ya César kama Julia Roberts, Christopher Nolan, Kevin Costner, George Clooney na Quentin Tarantino.
Mashabiki wake walioona picha zake mitandaoni walishangaa alichofanyia uso wake huku wengine wakiamini kwamba alifanyiwa upasuaji wa kuuboresha almaarufu ‘botox’.
Baada ya kupokezwa tuzo, Carrey alitoa hotuba fupi katika lugha ya kifaransa hali iliyoshangaza mashabiki hata zaidi kwani hawakufahamu anajua kuzungumza kifaransa.
Alifichua kwamba ana asili ya kifaransa kwani babu yake aitwaye Marc-François Carré, alizaliwa katika eneo la Saint-Malo, nchini Ufaransa kabla ya kuhamia Canada, karne kadhaa zilizopita.