Mwanamuziki wa China Ferren Lee maarufu kama Coco Lee ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 48.
Dada zake wakubwa Carol na Nancy ndio walitoa taarifa hiyo kupitia Instagram.
Wawili hao walielezea kwamba dada yao amekuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa muda mrefu na alijaribu kujitoa uhai Jumapili iliyopita, akapelekwa hospitali na akaaga jana Jumatano.
Lee, ambaye alilelewa huko California, Amerika, alifanya bidii sana kutangaza muziki wa China katika jukwaa la ulimwengu.
Mnamo mwaka 2001, alitambuliwa na waandalizi wa tuzo za Oscar ambapo aliimba wimbo wake bora asilia na kuandikisha historia ya mwanamuziki wa kwanza wa asili ya China kuwahi kutumbuiza kwenye tuzo za Oscar.
Lee alianza kazi kama mwanamuziki akiwa na umri mdogo baada ya kuibuka mshindi kwenye shindano la uimbaji lililoandaliwa na kituo cha utangazaji cha TVB.
Mwaka 1994, alitoa albamu yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 19 pekee.
Alianza kuimba kwa lugha ya Kichina, lakini baadaye akaimba lugha nyingine kama vile Kiingereza.
Mwaka 1999, Lee alitoa albamu yake ya kwanza ya lugha ya Kiingereza kwa jina “Just No Other Way”.
Aliolewa na mfanyabiashara wa Canada Bruce Rockowitz mwaka 2011 ila hakujaliwa watoto.
Mume wake hata hivyo ana mabinti wawili kutoka kwa ndoa yake ya awali.