Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Raila Odinga, umewasili Jijini Kisumu kutoa fursa kwa wakazi wa Nyanza kuutazama.
Ndege ya kijeshi iliyokuwa imeubeba mwili wa Raila, ilitua katika uwanja wa ndege wa Kisumu muda mfupi baada ya saa mbili asubuhi.
Baadaye mwili huo ulibebwa kwa ndege aina ya helikopta ya jeshi hadi katika uwanja wa Mamboleo.
Wananchi wamejaa sisi kwenye uwanja wa Mamboleo, wakijitokeza kushiriki shughuli ya umma ya kuutazama mwili wa Raila Odinga.
Viongozi wa Nyanza wakiwemo Magavana, Wabunge na Wawakilishi wadi wanahudhuria zoezi la kuutazama mwili huo.
Kabla ya umma kuutazama mwili huo, viongozi wa dini wataongoza kipindi kifupi cha maombi.
Baada ya shughuli ya kutazama mwili kukamilika Jumamosi jioni, mwili huo utapelekwa kukesha usiku kucha nyumbani kwa Raila Odinga Bondo, kaunti ya Siaya.
Raila Odinga aliyefariki Jumatano akipokea matibabu nchini India, atazikwa Jumapili katika makaburi ya familia ya Kang’o ka Jaramogi.
 
					 
				 
			
 
                                
                              
		 
		 
		 
		