Mwijaku ammiminia mkewe sifa kama njia ya kuzima uvumi kumhusu

Hii ni baada ya video ya wasichana wawili wanaompigania kusambaa mitandaoni.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamitandao na mtangazaji wa Tanzania Burton Mwemba maarufu kama Mwijaku, ameamua kummiminia mke wake sifa kama njia ya kuzima uvumi kumhusu unaoendelea mitandaoni.

Haya yanajiri baada ya video kuvujishwa mitandaoni inayoonyesha wasichana wawili wanaodaiwa kuwa wanafunzi wa chuo kikuu wakipigana kisa na sababu Mwijaku.

Mmoja wa wasichana hao anayefahamika kama Mary, anasikika akimfokea mwingine akimtaka aelezee wakati ambapo alikutana na Mwijaku ambaye anamrejelea kuwa mpenzi wake.

Mary alikuwa na mori kiasi cha kukata msichana huyo mwingine nywele kwa madai ya kumpokonya mpenzi.

Sasa katika akaunti yake ya Instagram, Mwijaku amechapisha picha za pamoja na mke wake za zamani na za sasa na kuandika, ” Wakati Adam anaumbwa alikuwa peke yake. Mungu hakumpa Video game acheze kusema litampa company. Mungu hakumpa marafiki kusema watampa furaha na kumsupport..bali alimpa Mke..Eva..ili awe msaidizi wake kwa kila jambo.”

Aliendelea kusema kwamba hatua alizochukua Mungu zinaonesha umuhimu wa kuwa na mwenzako wa maisha katika hali zote .

“Marafiki watakuja na kuondoka, watoto watakua na kwenda kuanzisha familia zao, wafanyakazi wenzako wataondoka, majirani watahama.” aliandika mtangazaji huyo akiongeza kwamba atakayesaia ni mwanandoa mwenzako ambaye mtatenganishwa tu na kifo.

Mwemba alihimiza wafuasi wake wawapende wapenzi wao kwa dhati na kuwepusiha ibilisi na vikwazo.

“Naamini hakuna kitu na hakuna mtu wa kuvunja ndoa yoyote ile labda Mungu mwenyewe apende . Iwe jua au iwe mvua ninakupenda Alice. Haijalishi nitaonekanaje lakini wewe ndio nguvu yangu na unajua hilo.

Mwijaku alimalizia kwa kusema, “Ndoa iliyofanikiwa sio umoja kati ya watu kamilifu. Ni muungano wa watu wawili wasio wakamilifu ambao wamefahamu thamani ya msamaha na neema.”

Kisa cha mabinti hao wa chuo kikuu kimetikisa Tanzania huku baadhi ya viongozi serikalini wakihimiza uongozi wa chuo husika utekeleze uchunguzi na kuchukua hatua.

Share This Article