Kesi inayomkabili mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA Tundu Lissu inatarajiwa kuendelea asubuhi ya leo katika mahakama ya hakimu huko Kisutu, Dar es Salaam.
Usalama tayari umeimarishwa katika eneo la mahakama hiyo ambapo Lissu anakabiliwa na kesi mbili, moja ya uhaini na nyingine ya kusambaza habari zisizo za kweli.
Wote ambao wamekuwa na ari ya kufuatilia kesi iyo sasa wana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu jana, mahakama ya Tanzania ilitangaza kwamba matukio yote ya kesi hiyo leo yatapeperushwa mubashara.
Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano katika idara ya Mahakama nchini Tanzania, Gerard Julius Chami, alisema lengo la urushaji wa matangazo ya moja kwa moja kutoka mahakamani leo ni kuruhusu kila mmoja kuifuatilia popote alipo.
Kulingana naye hatua hiyo inatarajiwa pia kupunguza msongamano wa watu katika eneo la mahakama ya Kisutu ambayo ina uwezo wa kumudu watu 80 pekee.
Nafasi hizo zimegawanyiwa wahusika wakuu wa kesi hiyo ambao ni Mawakili wa Serikali na Watu wengine 10, Mawakili wa utetezi na Watu wengine 60 na Waandishi wa habari 10.
Haya yanajiri wiki mbili baada ya wanaharakati wa Kenya na Uganda kufurushwa Tanzania ambapo walikuwa wamekwenda kwa ajili ya kufuatilia kesi ya Lissu.
Siku hiyo kesi hiyo haikuendelea kutokana na hatua ya upande wa serikali kusema kwamba haukua umekamilisha uchunguzi.
Mashtaka yanayomkabili kiongozi huyo wa upinzani yanatokana na kampeni ya chama chake ya kutaka mabadiliko yafanywe kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa Oktoba mwaka huu.