Mwigizaji Johnny Depp kutoa pesa zote alizolipwa na aliyekuwa mke wake kwa usaidizi wa jamii

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa Marekani John Christopher Depp II maarufu kama Johnny Depp ameamua kutoa pesa zote alizolipwa na aliyekuwa mke wake Amber Heard baada ya kesi ya kumharibia sifa kama mchango kwa usaidizi wa jamii. Depp alilipwa Dola milioni moja na Amber baada ya kushinda kesi hiyo mwaka jana.

Kulingana na jarida la People Depp atagawa pesa hizo kwa mashirika matano ya usaidizi wa jamii ambapo kila moja litapokea Dola laki mbili. Mashirika hayo ni Make-A-Film Foundation, The Painted Turtle, Red Feather, Tetiaroa Society na Amazonia Fund Alliance.

Depp aliweka kesi ya kuharibiwa sifa mahakamani mwezi Machi mwaka 2019 akidai fidia ya Dola milioni 50 baada ya jarida la Washington Post kuchapisha makala yaliyoandikwa na Amber akielezea alivyodhlumiwa katika ndoa. Ingawa hakutaja jina la Depp kwenye makala hayo, yalichapishwa wakati ambapo talaka yao ya mwaka 2016 ilikuwa bado inazungumziwa.

Mwezi Juni mwaka 2022, jopo la waamuzi lilimpendelea Depp na kumzawadi Dola milioni kumi kama fidia ya kuharibiwa sifa. Jopo hilo la waamuzi lilimwongezea Dola milioni 5 kama fidia ya adhabu lakini ikapunguzwa hadi Dola 350 000 kuambatana na kiwango cha juu zaidi cha fidia hiyo kilichowekwa na serikali.

Hata baada ya kumpa ushindi Depp, jopo hilo hilo la waamuzi lilimpata Depp na hatia kufuatia matamshi ya wakili wake Adam Waldman. Wakili huyo alikuwa ametaja madai ya Amber kuwa uwongo na hivyo wakatozwa fidia ya Dola millioni 2.

Website |  + posts
Share This Article