Mwigizaji Jay North afariki

Rafiki yake aitwaye Laurie Jacobson, alisema kwamba Jay alifariki Jumapili nyumbani kwake huko Lake Butler, Florida baada ya kuugua saratani ya utumbo.

Marion Bosire
4 Min Read

Mwigizaji Jay North mhusika mkuu wa kipindi cha televisheni cha miaka ya 1960 “Dennis the Menace” amefariki akiwa na umri wa miaka 73.

Habari hizi zilitolewa na Laurie Jacobson rafiki yake wa wa muda mrefu ambaye pia ni mke wa mwigizaji Jon Provost aliyesema kwamba Jay alifariki Jumapili nyumbani kwake huko Lake Butler, Florida baada ya kuugua saratani ya utumbo.

Afya yake ilianza kuzorota mwezi mmoja uliopita na alikuwa na familia yake — mkewe Cindy na binti zake kutoka kwa ndoa ya awali, ambao aliwapenda sana.

Laurie anasema Cindy na binti zake walimpa familia ambayo hakuwahi kuwa nayo kwani alikuwa mtoto pekee ambaye hakuwahi kumfahamu babake.

Jay alikuwa hajaona marafiki zake kwa muda kwa sababu alijitenga kutunza afya yake alipokuwa akiugua saratani.

Lakini, Laurie alikusanya barua nyingi kutoka kwa mashabiki na marafiki ambazo alimpelekea wakati wa Krismasi — jambo ambalo anasema lilimfurahisha sana.

North alijulikana sana mwishoni mwa miaka ya 1950 … akionekana katika sehemu ndogo kwenye vipindi kama “77 Sunset Strip,” “Rescue 8,” na “Sugarfoot” wakati alikuwa na umri chini ya miaka 10.

Jay alijulikana kitaifa mwaka 1959 alipoanza kucheza kama Dennis Mitchell katika “Dennis the Menace”… akiongoza vipindi vyote 146 kutoka 1959 hadi 1963.

Nywele zake zilifanywa kuwa rangi ya platinum blonde kwa ajili ya sehemu hiyo, na alielekezwa kusema kuwa alikuwa mdogo kwa mwaka mmoja kuliko alivyokuwa katika mahojiano.

North aliwahi kusimulia kwamba alipitia shida nyingi kwenye maandalizi ya kipindi cha Dennis The Menace miaka mingi baada ya kipindi hicho kumalizika.

Alidai kwamba shangazi yake alimrushia maneno makali na hata kumdhulumu kila alipokosea maneno ya uigizaji. Nyakati zingine alikuwa akimchukua mbali na macho ya watu ili ampige kwa kukosea huko.

Jay alitetea mamake mzazi na wengine waliokuwa wakihusika katika maandalizi ya kipindi akisema hawakuwa na habari kuhusu unyanyasaji huo wakati huo.

Jacobson naye alithibitisha kwamba alikuwa na wakati mgumu Hollywood na hakufurahia aliyoyapitia jambo lililosababisha awe na hasira na chuki kubwa wakati huo kwa sababu watu wazima waliomzunguka hawakufanya chochote kumsaidia au kufanya kazi yake na maisha yake kuwa rahisi.

Kipindi cha Dennis the Menace kilikomeshwa baada ya misimu minne na baada ya hapo North aliangazia uigizaji wa sauti pekee mwisho wa miaka ya 1960 na mwanzo wa miaka ya 70 katika kazi kama “Arabian Knights,” “Here Comes the Grump,” na “The Pebbles and Bamm-Bamm Show.”

Mwisho wa miaka ya 1980, North aliacha uigizaji, huku akihusishwa kwa uchache katika kipindi cha “The Simpsons” na katika filamu ya David Spade “Dickie Roberts: Former Child Star.”

Katika miaka ya hivi karibuni, North alifanya kazi kama afisa wa magereza huko Florida ambapo alikuwa anasaidia vijana wenye shida katika mfumo wa watoto wahalifu.

Alisaidia pia kuwaunganisha na nyota wa zamani wa utotoni kupitia kundi la A Minor Consideration katika miaka ya 1990.

Jacobson anasema pia kwamba alifanya kazi na wafungwa waliohukumiwa kifo ambao walikuwa na nyakati ngumu utotoni na mazungumzo yao yalimsaidia kupata amani na miaka yake ya utoto.

Licha ya kutoipenda Hollywood, Jacobson anasema Jay alikubali faida moja aliyopata kutoka kwa sekta hiyo ambay ni marafiki wa maisha yote ambao walikuwa pia nyota wa utotoni wakati mmoja, akiwemo Angela Cartwright, Jerry Mathers, Stan Livingston, Paul Petersen, na Brandon Cruz, miongoni mwa wengine.

Website |  + posts
Share This Article