Mwanga wa Gavana Mwangaza wazimwa na Mahakama Kuu

Martin Mwanje
1 Min Read
Kawira Mwangaza - Gavana wa Meru

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kudumisha uamuzi wa Bunge la Seneti wa kumfurusha madarakani. 

Gavana Mwangaza alielekea mahakamani kupinga uamuzi huo akidai Seneti haikufuata utaratibu unaofaa katika kumfurusha.

Hata hivyo, Jaji Bahati Mwamuje leo Ijumaa asubuhi amepuuzilia mbali madai ya Gavana huyo wa Meru akisema Seneti haikukosea abadan katika kumtema.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwamuye alisema Gavana Mwangaza alipewa fursa kujitetea dhidi ya mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake katika Bunge la Seneti na isitoshe aliwakilishwa na mawakili.

Kulingana na Jaji huyo, mahakama haina msingi wa kuingilia utendakazi wa Seneti au Bunge la Taifa.

Maseneta wengi walipiga kura mwaka jana kuidhinisha mashtaka yaliyowasilishwa na Bunge la kaunti ya Meru likitaka lMwangaza abanduliwe madarakani.

Mashtaka hayo yalijumuisha matumizi mabaya ya mamlaka na ubadhirifu wa rasilimali za kaunti.

Tangu kuteuliwa kwake, Gavana Mwangaza amekuwa akilumbana na wawakilishi wadi na viongozi wengine wa kaunti ya Meru katika kile ambacho Gavana huyo amedai kimetokana na mfumo wa ubaba dume uliokitihiri katika kaunti hiyo.

Gavana Mwangaza ameitaka mahakama kuzuia utekelezaji wa uamuzi huo kwani ana kusudi la kukata rufaa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *