Mwanamuziki wa kike wa Tanzania Haitham Kim ameaga dunia siku chache tu baada ya kuugua. Alikata roho akiendelea kupata matibabu katika hospitali ya rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Siku chache kabla ya kifo chake, mume wake na wanamuziki wenza walikuwa wameanzisha harakati za kuchangisha pesa zakugharamia matibabu kupitia mitandao.
Harmonize, Alikiba, Nandy na wanamuziki wengine wa Bongo walikuwa wametangaza mchango huo kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii.
Mumewe Haitham kwa jina Bryson Peter Mtei alitoa namba yake ya simu ya rununu kwa ajili ya kutumiwa michango akisema Haitham alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Binti huyo alilazwa hospitalini akiwa na dalili za ugonjwa wa pumu ambao ulikithiri na kusababisha kifo chake.
Mwili wa marehemu Haitham uliondolewa hospitalini Temeke na kupelekwa kwenye msikiti wa Upanga kuandaliwa kwa mazishi.
Mwana FA au ukipenda Hamisi Mwinjuma ambaye ni mbunge na naibu Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo amefika msikitini humo kwa ajili ya kufariji waliofiwa.
Alihojiwa na wanahabari akiwa eneo hilo ambapo alisema aliwahi kushirikiana na Haitham kwenye wimbo mmoja ndio sababau anamfahamu.