Mvua za El Nino: Serikali kuhakikisha mitihani ya kitaifa haitaathiriwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Katibu wa Elimu ya Msingi Dkt. Belio Kipsang

Serikali imetangaza mipango ya kutumia ndege kutoa usaidizi katika maeneo yatakayokumbwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha nchini wakati wa mitihani ya kitaifa itakayofanyika kuanzia mwezi Novemba.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini imetangaza kuwa mvua za El Nino zinatarajiwa kunyesha nchini kati ya mwezi Oktoba hadi Disemba.

Kuna hofu kuwa mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha wakati wa kipindi hicho huenda zikaathiri pakubwa usimamizi wa mitihani ya kitaifa ya KCPE, KPSEA na KCSE.

Huku akifahamu bayana athari zinazoweza kutokana na mvua hizo, Katibu wa Elimu ya Msingi Dkt. Belio Kipsang anasema wanafanya kazi na maafisa wengine wa serikali wakiwemo makamishna wa kikanda na kaunti kubaini maeneo yatakayokumbwa na mvua hizo.

“Tunajiandaa kwa mtihani wakati ambapo mvua za El Nino zinatarajiwa. Tutabaini maeneo yatakayokumbwa na mafuriko na kuweka mipango ya kuhakikisha wasimamizi wa mitihani wanafika katika vituo vya kufanyia mitihani hiyo kwa wakati unaofaa,” alisema Dkt. Kipsang.

“Kwa pamoja, tunafanya kazi kukusanya vifaa vyote vilivyopo serikalini ikiwa ni pamoja na helikopta zetu za polisi, jeshi, huduma ya misitu na KWS, vifaa vyote hivyo tutavitumia kuwasaidia watoto wetu wakati wa mtihani.”

Dkt. Kipsang aliyasema hayo wakati wa mkutano na maafisa wa elimu kutoka eneo la Pwani uliofanyika katika shule ya upili ya Shimo la Tewa jijini Mombasa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na makamnisha wote sita wa kaunti na manaibu wao, wanachama wa timu za usalama za eneo hilo na maafisa kutoka chama cha walimu nchini KNUT miongoni mwa wengine.

Dkt. Kipsang alisisitiza utayari wa serikali kusimamia mitihani hiyo na kuwahakikishia wanafunzi kuwa serikali imeweka mikakati kabambe kuhakikisha mitihani hiyo haitatatizika kutokana na mvua hizo.

Wanafunzi wapatao milioni 3.5 wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa mwaka huu.

Takriban wanafunzi milioni 1.4 watafanya mtihani wa KCPE, wengine milioni 1.2 mtihani wa KPSEA na wanafunzi wapatao 900,000 watafanya mtihani wa KCSE.

Share This Article