Leo Jumatatu imekuwa siku ya kipekee katika ulingo wa kisiasa ambapo muungano mpya wa kisiasa umetangazwa kuzaliwa.
Na wakati ujio wa muungano huo ukibainika, muungano wa Azimio ambao awali uliwaleta pamoja vyama vya ODM, Wiper, DAP-K, Jubilee na Narc K umeonekana kuzikwa katika kaburi la sahau.
Muungano mpya uliotangazwa wakati wa kuzinduliwa kwa makao makuu ya DAP-K unawaleta pamoja aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper, Jeremiah Kioni wa chama cha Jubilee na Martha Karua wa chama cha Narc K.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka na Seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malalah pia wamejiunga na muungano huo ambao jina lake linatarajiwa kutangazwa siku zijazo.
Gachagua ameashiria kuwa atatangaza kubuniwa kwa chama chake kipya baada ya kufurushwa kutoka chama cha UDA.
Wakizungumza wakati wa kuzinduliwa kwa makao makuu mapya ya chama cha DAP-K, Kalonzo na Gachagua walielezea imani kwamba watambwaga Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Gachagua, hususan aliwataka viongozi wa upinzani kudumisha umoja na kutokubali maslahi ya kibinafsi kuwagawanya.
Rais Ruto ameelezea imani kuwa yuko tayari kukabiliana na mahasimu wake wa kisiasa katika uchaguzi ujao, akisema ana imani ya kuhifadhi kiti chake.
Ruto ameonekana kuungana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuelekea uchaguzi huo, na wabunge wanaogemea upande wa Raila, wamekuwa wakimuunga mkono Rais tangu kuteuliwa kwa baadhi yao kuwa Mawaziri.