Mutua atetea kufutwa kwa wafanyakazi wa viwanda vya sukari

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Leba na utunzaji wa jamii Dkt. Alfred Mutua, ametetea kufutwa kazi kwa baadhi ya wafanyakazi wa viwanda vya serikali vinavyomilikiwa na serikali, vilivyobinafsishwa maajuzi.

Akizungumza katika bunge la Seneti leo alipokuwa akijibu maswali yaliyoibuliwa na maseneta, Mutua alielezea kwamba hatua hiyo ni sehemu ya mpango unaolenga kurejesha ufanisi, uendelevu na ushindani katika sekta ya sukari.

Mutua alikabiliwa na maswali ya Seneta wa Kisumu Tom Ojienda yaliyosomwa na Seneta mteule Beatrice Ogolla kwa niaba yake, kuhusu mageuzi katika viwanda vya serikali vya sukari na nguo.

Kulingana na Mutua, hatua zinazochukuliwa na serikali zimeongozwa na sheria na heshima kwa wafanyakazi.

Gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Machakos alisema mchakato wa kutambua wafanyakazi wasiohitajika na kuwafuta ulitekelezwa kwa mujibu wa sehemu ya 40 ya sheria ya ajira.

Sehemu hiyo inawataka waajiri kufahamisha vyama vya wafanyajkazi husika na wafanyakazi walioathirika kuhusu hatua hiyo, kuihalalisha na kuwalipa malimbikizi yao kulingana na mkataba wa ajira.

Chama cha wafanyakazi wa mashamba ya miwa awali kilikwenda kortini kusimamisha kufutwa kazi kwa wafanyakazi hao hadi mustakabali wao uthibitishwe.

Hata hivyo Mutua alifichua kwamba wizara ya kilimo, bodi ya sukari ya Kenya na wizara ya fedha zilishauriana na chama hicho cha wafanyakazi na wakaafikia mapatano Mei 7, 2025, ambayo yangeongoza mchakato huo.

Wafanyakazi 1,743 wameathiriwa na mageuzi katika viwanda vya sukari vya Chemelil, Muhoroni na Miwani katika kaunti ya Kisumu.

Website |  + posts
Share This Article