Katibu wa afya ya umma katika wizara ya Afya Mary Muthoni amesema kwamba serikali inajitahidi kutekeleza mpango wa afya ya jamii almaarufu SHIF.
Muthoni ambaye alikuwa akizungumza katika kanisa la ACK huko Mburi eneo bunge la Gichugu alisema hakuna wasiwasi wowote na kwamba wakenya wanaweza kutumia kadi zao za NHIF kupata huduma za afya katika vituo vyote vya afya humu nchini.
Alisema hakuna yeyote atakayefukuzwa kutoka kwa kituo cha afya cha umma kwa vile kadi ya bima ya NHIF inafanya kazi kwa wakenya wote.
Muthoni aliongeza kwamba pindi tu mpango wa SHIF utakapotekelezwa, wakenya ambao awali walikuwa wanalipa shilingi-500 sasa watalipa shilingi-300 kila mwezi.
Muthoni pia alitahadharisha wakenya dhidi ya kuingiza siasa katika suala hilo huku akiwahimiza wawe na subira serikali inapoweka mikakati mwafaka ili iweze kuzindua bima hiyo ya matibabu.
Mpango wa bima ya afya wa SHIF unachukua mahali pa bima ya NHIF baada ya Rais William Ruto kutia saini sheria tatu kuhusu afya ambazo zinatoa fursa ya kuanzishwa kwa bima hiyo mpya.