Mabingwa watetezi wa kitaifa na Afrika mashariki wa mchezo wa magongo baina ya shule za upili Musingu, na mahasimu wao wa jadi St.Antony, watatifua kivumbi tena kesho Jumamosi katika fainali ya mashindano ya kitaifa yanayoendelea mjini Mombasa.
Musingu sawia na mwaka jana waliipepeta St. Charles Lwanga, magoli tatu kwa nunge nayo St. Antony ikawafunga Mpesa Academy, magoli tatu kwa moja kwenye nusu fainali.
Kwenye raga ya wachezaji 15 kila upande, wavulana wa Kisii na Vihiga watakabana koo baada ya kuwarambisha sakafu mabingwa watetezi All saints Embu alama 12 kwa 3, nayo Vihiga ikaipiku Upper Hill alama 10 kwa 8 katika nusu fainali nyingine.
Katika finali ya mpira wa vikapu wa wavulana, mabingwa watetezi Dr. Aggrey, watafanya juu chini kuhifadhi taji dhidi ya Laiser Hill.
Mabingwa hao walifuzu hatua hiyo walipowanyuka Lukenya School alama 70 kwa 66, nao Laiser wakapata ushindi wa alama 83 dhidi ya 79 za Dagoretti kwenye nusu fainali.
Upande wa vidosho pia mambo yalikuwa sawia ,mabingwa watetezi Butere wakifuzu kwa fainali walipowacharaza Olimpic alama 62 kwa 35, na watachuana na Kaya Tiwi, waliowaponda St. Joseph, alama 62 kwa 40 wakati wa nusu fainali.