Museveni atishia kuwapa silaha walinzi wa mashinani ili kukabiliana na wezi wa Kahawa

Wizi wa zao la kahawa umekithiri sana nchini Uganda hasa kutokana na bei nzuri ya zao hilo.

Marion Bosire
1 Min Read
Yoweri Museveni, Rais wa Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametishia kuwapa silaha wanachama wa makundi ya ulinzi mashinani maarufu kama LDU, katika jitihada za kukabiliana na wezo wa mbuni za kahawa kwenye mashamba.

Wizi wa zao la kahawa umekithiri sana nchini Uganda hasa kutokana na bei nzuri ya zao hilo.

Kiongozi huyo wa Uganda aliyasema hayo katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka na ya kukaribisha mwaka mpya akiwa nyumbani kwake katika eneo la Rwakitura.

Rais Museveni alionyesha kughadhabishwa kwake na hatua ya wezi wengine ya kuiba mbuni ambazo hazijakomaa, akisema wanatishia ubora wa kahawa ya Uganda hasa katika masoko ya kimataifa.

Alisema pia kwamba katika harakati za kuiba zao hilo, wezi huharibu mikahawa na hivyo kutishia mustakabali wa uzalishaji wa zao hilo.

Museveni alitoa mfano wa ripoti ya hivi karibuni ya jeshi la Uganda UPDF ambapo wakulima walipatikana wakivuna mbuni ambazo hazijakomaa.

Katika kujitetea wakulima hao walisema waliamua kufanya hivyo kama njia ya kuokoa zao hilo kutokana na wezi, hatua inayotishia pia ubora wa kahawa ya Uganda.

Huku akitaja wakulima wa kahawa kuwa miongoni mwa wanaoiletea Uganda mapato, Museveno alisema kwamba wahusika wasipokomesha uovu huo, atatumia jeshi kutoa silaha kwa LDU ili kuhakikisha ulinzi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *