Musalia Mudavadi ateuliwa kukaimu nyadhifa zote za mawaziri

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ameteuliwa kukaimu nyadhifa zote za mawaziri.

Nyadhifa zote 21 ziliachwa wazi baada ya Rais William Ruto kuvunja Baraza lake la kwanza la Mawaziri tangu alipoingia madarakani.

Hata hivyo, Mudavadi ambaye pia ni kinara wa mawaziri alisazwa kwenye hatua hiyo ambayo imeungwa mkono na Wakenya wengi.

Katika gazeti rasmi la serikali leo Jumatano, Rais Ruto ametangaza kumteua Mudavadi kukaimu nyadhifa zote za mawaziri waliopigwa kalamu.

“Kuambatana na sehemu ya 52(5)(a) ya katiba, Wycliffe Musalia Mudavadi ameteuliwa kukaimu nyadhifa zote za mawaziri,” alisema Rais Ruto kupitia gazeti hilo rasmi la serikali.

Alipovunja Baraza la Mawaziri, Rais Ruto alisema hatua hiyo ililenga kufanyia mageuzi serikali yake, ili kufanikisha utoaji huduma kwa wananchi.

Kiongozi huyo wa taifa alisema atabuni baraza jipya la mawaziri litakalomsaidia kutekeleza ajenda za serikali zikiwemo kudhibiti deni la kitaifa, kuimarisha mapato, kubuni ajira, kukomesha utumizi mbaya wa raslimali na ushirikishaji wa majukumu miongoni mwa mashirika ya serikali.

Website |  + posts
Share This Article