Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesikitikia mauaji yaliyotokea katika eneo la Angata Barrikoi, Transmara, kaunti ya Narok, akithibitisha kuwa uchunguzi umeanzishwa kuwatambua waliopanga ghasia hizo siku ya Jumatatu.
Ghasia zilizuka katika eneo hilo kutokana na mzozo wa ardhi, ambapo maafisa wa polisi walikabiliana na wananchi na kusababisha maafa hayo.
“Natuma risala za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao wakati wa ghasia hizo zilizotokea katika eneo la Ang’ata Barrikoi,” alisema kupitia kwa taarifa.
“Ninasikitika kuwa hali hiyo ilisababisha kupotea kwa maisha ya maafisa wa polisi na raia. Uchunguzi unaendelea kuthibitisha idadi kamili ya maafa.” aliongeza waziri huyo.
Murkomen aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo kwamba, licha ya wao kuwa na wasiwasi, hakuna atakayepoteza ardhi yake, akiwataka kuwa watulivu serikai inaposhughulikia swala hilo.
“Kwa wakazi wa eneo hilo tunawahakikishia kwamba hakuna yeyote atachukua ardhi yao chini ya serikali hii, hakuna haja ya wao kuchukua sheria mikononi mwao,” alidokeza waziri Murkomen.
Aidha waziri huyo alidokeza kuwa usalama umeimarishwa katika eneo hilo akihimiza kuwepo kwa hali ya utulivu.