Serikali hadi kufikia sasa imewahamisha wakenya 35 kutoka taifa linalokabiliwa na machafuko Lebanon, kulingana na waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.
Akiwahutubia wanahabari leo Alhamisi, Mudavadi alithibitisha kuwa Makundi mengine mawili ya wakenya, yataondolewa nchini humo mwishoni mwa wiki hii.
Mudavadi alisema hali nchini Lebanon si salama, kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas, ambavyo vimepenyezwa hadi Lebanon.
“Hapaswi kuhatarisha maisha yao, si mzaha huko,” alisema Mudavadi.
Wakati huo huo, Mudavadi alisema hakuna mkenya amejeruhiwa nchini Lebanon.
Kulingana na Mudavadi ambaye pia ni waziri wa Mambo ya Nje, kati ya wakenya 26,000 nchini Lebanon, ni 7,119 pekee ambao wamejisajili kuhamishwa, licha ya hali ya wasiwasi inayoshuhudiwa nchini humo.
Aidha alisema serikali imebuni kundi la taasisi mbali mbali la kuwaondoa wakenya nchini Lebanon.
“Tunashirikiana kwa karibu na ubalozi wa Kenya nchini Kuwait, uongozi wa Kenya nchini Lebanon, serikali ya Lebanon, shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na mashirika mengine yasiyo ya serikali kuhakikisha mchakato shwari wa kuwahamisha wakenya,” alisema Mudavadi.
Waziri Musalia amewahimiza wakenya zaidi wajisajili ili kurahisisha shughuli ya kuwaondoa kutoka nchini humo.
Lebanon imekuwa ikishambuliwa na jeshi la Israel tangu ilipoanza kuwashambulia wapiganaji wa kundi la Hezbollah mwezi uliopita.