Mudavadi: Serikali inajizatiti kuwaokoa Wakenya waliokwama Urusi

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.

Serikali imesema inafuatilia habari za vyombo vya habari kuhusu Wakenya wanaodaiwa kukwama katika mapigano baina ya Urusi na Ukraine.

Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, alisema serikali kupitia wizara hiyo imeshauriana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi katika juhudi za kuachiliwa salama kwa raia wa Kenya wanaotatizika na kuhakikisha wanasafiri salama kurejea nyumbani.

Musalia alisema maafisa wa Kenya na Urusi walifanya mkutano muhimu mwezi uliopita ambapo walielezea haja ya Wakenya, wakiwemo wanaozuiliwa katika kambi mbalimbali za kijeshi katika taifa la Urusi, kufika kwenye ubalozi wa Kenya mjini Moscow, ambako itakuwa rahisi kwa serikali kupanga usafiri wao kuja nyumbani.

Alisema mataifa hayo mawili yalikubaliana kwamba wale wanaozuiliwa bila hiari yao wanapaswa kukabidhiwa ubalozi wa Kenya mjini Moscow haraka iwezekanavyo.

Kulingana na Mudavadi, Kenya imeelezea wasiwasi kuwa vijana wa hapa nchini wanahadaiwa na mawakala watundu kusafiri Urusi na bila kujua, wanajipata katika kambi za kijeshi.

Alisema ubalozi wa Kenya nchini Urusi umeanzisha harakati kubainisha idadi kamili ya Wakenya wanaozuiliwa katika kambi za kijeshi za Urusi, kwa lengo la kuwarejesha nyumbani.

Website |  + posts
Share This Article