Mudavadi ataka ahadi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutimizwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Afrika inasalia kuwa moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi anasema hii ni licha ya kwamba bara hili limetoa mchango mdogo mno kwa uzalishaji wa sasa na wa kihistroia wa gesi chafuzi kwa mazingira duniani.

Mudavadi amelalama kuwa licha ya kwamba licha ya Afrika kuwa mstari wa mbele katika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi, ilipokea tu asilimia 20 pekee ya fedha za kukabiliana na mabadiliko hayo. Hii ni sawa tu na dola bilioni 13 za Marekani katika kipindi cha miaka ya 2021–2022.

“Mataifa mengi ya Afrika yanakabiliwa na athari kubwa zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, zinazochangiwa mno na ukosefu wa ufadhili wa kutosha na rasilimali za kiufundi,” alisema Mudavadi aliyezungumza wakati wa tukio la Siku ya Afrika kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi wa COP29 unaoendelea nchini Azerbaijan.

“Inasikitisha kuwa, ahadi za dunia za kutoa ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hazijakuwa za kutosheleza, zikiwa na upungufu wa kinachohitajika kwa dharura.” 

Kinara huyo wa Mawaziri ametoa wito kwa viongozi wa dunia kutosahahu ahadi ambayo haijatimizwa ya dola bilioni 100 kwa mwaka iliyotolewa mwaka wa 2009.

Mudavadi aliyeandamana na Mawaziri Aden Duale wa Mazingira na Opiyo Wandayi wa Nishati, miongoni mwa maafisa wengine serikalini, anamwakilisha Rais William Ruto kwenye mkutano huo.

 Kulingana naye, ahadi hizo wakati huu zinapaswa kuambatana na vitendo.

Share This Article