Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje ameimarisha juhudi za kuinadi Kenya kidiplomasia katika mataifa mbalimbali duniani.
Jana Jumatatu, alikutana na mabalozi mbalimbali kutoka Umoja wa Ulaya, EU waliotumwa kuhudumu Nairobi kama sehemu ya mkakati wa nchi hii kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande nyingi.
Mudavadi anasema mkutano huo uliangazia kuhamasisha kwa njia endelevu hatua inayopigwa katika majadiliano hasa yanayohusu biashara na uwekezaji wakati Kenya ikitafuta kuongeza kiwango cha bidhaa zinazouzwa kwenye soko la EU.
Aliwahakikishia mabalozi hao kuwa nchi hii imekusudia kuhakikisha matumizi bora ya fedha ikiwa ni pamoja na kukabiliana na jinamizi la ulanguzi wa fedha na ufadhili wa ugaidi.
Kadhalika, Mudavadi aliwataarifu mabalozi hao juu ya mipango na matayarsho yanayoendelea kwa Kenya kuandaa mkutano wa Umoja wa Maendeleo Duniani wa Benki ya Dunia (IDA21)2024.
Anasema mkutano huo utatoa jukwaa muhimu la kufanya majadiliano ya kuleta mageuzi duniani, ikiwa ni pamoja na kujenga mbinu na miundo bunifu ya ufadhili duniani.