Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ameelekea nchini Angola ili kuhudhuria Mkutano Usiokuwa wa Kawaida wa Baraza la Umoja wa Afrika, AU uliopangwa kufanywa Agosti 30, 2026.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje atamwakilisha Rais William Ruto kwenye mkutano huo.
Mkutano huo utatafuta njia za kuimarisha mbinu za kuzuia migogoro na utatuzi wake barani Afrika.
“Mazungumzo yanatarajiwa kuzingatia hatua za kivitendo za kuongeza uwezo wa bara, kuzuia, kusimamia na kutatua migogoro,” ilisema taarifa kutoka kwa Ofisi ya Mudavadi.
Mudavadi pia atatumia mkutano huo kuendeleza utangamano wa kikanda na ajenda ya maendeleo ya pamoja ya Afrika wakati Kenya ikiendelea kuimarisha ushawishi wake ndani ya AU.
Kenya inashiriki Mkutano Usiokuwa wa Kawaida wa Baraza la AU wakati ambapo imepata hadhi ya Daraja la Kwanza ndani ya AU.
Mudavadi ametaja hatua hiyo kuwa muhimu akisema itasaidia kuimarisha sauti na ushawishi wa Kenya katika Umoja wa Afrika.