Mtumishi asimulia uhusiano uliozorota kati yake na mamake mzazi

Marion Bosire
2 Min Read

Mchekeshaji Mtumishi wa kundi la wawili maarufu kama mchungaji na mtumishi ambaye jina lake halisi ni Gilbert Baraza ameshangaza wengi baada ya video yake akikiri kutomjali mamake kusambaa mitandaoni.

Msanii huyo alikuwa akizungumza kwenye kanisa moja ambako alisimulia jinsi amekatiza uhusiano kabisa na mamake mzazi kutokana na visa vyake vilivyomuathiri.

Alielezea kwamba mama huyo alivunja ndoa kati yake na babake kwa kutumia ushirikina. “Nikiwa mdogo alikuwa ananipatia vitu niweke kwa mlango ndio baba akija avuke. Baba akija ninamwambia kwa sababu mimi ni mtoto sijui lolote, baadaye inakuwa vita.”

Aliendelea kusema kwamba alipoanza mambo ya kuchekesha nyumbani, mamake hakumuunga mkono kwani majirani walihisi kwamba huenda akageuka mwendazimu na hilo likasababisha mamake amfukuze nyumbani.

“Aliniambia toka na nisikuone kwa hii nyumba,” alisimulia mchekeshaji huyo.

Hapo ndipo alikopa mpenzi wake wa zamani elfu 5 akaanzisha biashara ya soseji barabarani huku akihudhuria mijarabu ya wachekeshaji wa kipindi cha Churchill.

Alipoanza kuonekana kwenye kipindi hicho ndipo wazazi wake ambao hawakumwaminia walianza kumuunga mkono.

Kilichokatiza uhusiano wake kabisa na mamake ni kuvunjika kwa ndoa yake ya miezi michache. Anasema baada ya harusi yake, mamake aliapa mbele ya babake kwamba ndoa hiyo haingedumu na ukweli haikudumu.

Anasema mama huyo hata akifa leo hataathirika kwa vyovyote kwa sababy ya machungu ambayo amemsababishia.

Share This Article