Msako dhidi ya bidhaa ghushi waimarishwa Taita Taveta

Tom Mathinji
1 Min Read
Kamishna wa Kaunti ya Taita Taveta Josephine Onunga.

Maduka mengi ya kuuza dawa za Binadamu na mifugo, baa na biashara ambazo hazina leseni kwenye Kaunti ya Taita Taveta, yamefungwa kufuatia msako dhidi ya bidhaa haramu uliotekelezwa na maafisa wa usalama wakiongozwa na kamishina wa kaunti hiyo,Josephine Onunga.

Hatua hii inajiri kufuatia amri ya waziri wa usalama wa taifa  Pro. Kithure Kindiki ya kutaka vitengo vya usalama kunasa madawa na pombe haramu kote nchini.

Kwa mujibu wa Onunga, walipata lita 1,000 za pasha, 2,500 za tangara, 5,000 za mbangara ,200 za changaa na zaidi ya watu 200 kutiwa mbaroni.

Aidha kamishna huyo aliongeza kuwa matumizi ya pombe yamezidisha visa vya unajisi, kuacha shule, talaka na kuvunjika kwa familia hivyo kusababisha watoto wengi wa mitaa na kuharibu ustawi wa taifa.

Vile vile amesema kuwa maeneo kama vile Voi na Mwatate yanachunguzwa.

Aliishukuru serikali ya kaunti hiyo, madhehebu na shule kwa ushirikiano wao dhidi ya vita hivyo.

Kwa upande wake, mkuu wa polisi wa kaunti hiyo Salid William alisema kuwa hawataruhusu biashara haramu na lazima kila mtu afuate sheria.

TAGGED:
Share This Article