Bingwa wa Dunia Mary Moraa na mshindi wa nishani ya fedha ya Afrika Amos Serem walitawazwa wa mwaka huu wa mashindano ya Diamond League katika siku ya kwanza ya mkondo wa mwisho wa Brussels,Ubelgiji Ijumaa usiku.
Serem,ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miakla 20 aliibuka mshindi wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, akimshinda bingwa wa Olimpiki na Dunia Soufiane El Bakkali wa Morocco ,katika jaribio la tatu na kumaliza utawala wa raia huyo wa Morocco ambaye alikuwa hajashindwa tangu Septemba mwaka 2021.
Serem aliongoza kutoka umbali wa mita 2,000 na kuibuka kidedea kwa kutumia muda wa dakika 8 sekunde 6.90,akifuatwa na El Bakkali katika nafasi ya pili kwa dakika 8 sekunde 8.60,mbele ya Mohammed Amin wa Tunisia, aliyeambulia nafasi na mshindi wa nishani ya shaba ya Olimpiki Abraham Kibiwott wa Kenya aliyeridhia nafasi ya nne.
Moraa alikamilisha msimu kwa nji ya kipekee akiibuka mshindi kwa kuziparakasa kwa dakika 1 sekunde 56.56 .
Mwingereza Georgia Bell alifuata katika nafasi ya pili, akifuatwa na Natoya Goule wa Jamaica katika nafasi ya tatu.
Timothy Cheruiyot alimaliza wa pili katika mita 1500, akitumia dakika 3 sekunde 30.37 nyuma ya Jakub Ingebrigsten wa Norway,aliyejizoa baada ya kukosa nishani katika michezo ya Olimpiki.
Berihu Aregawi aliwaongoza Waethiopia kunyakua nafasi tatu za kwanza katika mita 5,000 huku Mkenya Nicholas Kimeli akimaliza wa nne.
Bingwa wa Olimpiki Julien Alfred wa visiwa vya Saint Lucia alimwabwaga tena bingwa wa Dunia Sha Carri Richardson wa Marekani, katrika mita 100 akitimka kwa sekunde 10.88 mbele ya Dinah Asher Smith wa Uingereza na Marie Jose Talou wa Ivory coast, walionyakua nafasi za pili na tatu katika usanjari huo.
Ackeem Ackeem Blake wa Jamaica alishinda mbio za wanaume kwa sekunde 9.93,mbele ya Wamarekani Christian Coleman na Fred Kerly, waliochukua nafasi za pili na tatu mtawalia.
Mashindano hayo yatakamilika Jumamosi usiku huku Wakenya wakishiriki fainali za mita 800 wanaume mita 1500 wanawake ,mita 3,000 kuruka viunzi na maji wanaeake na mita 5,000 wanawake.
Washindi wa kila fani watatuzwa shilingi milioni 3.9 ,tuo ya Almasi na tiketi ya kushiriki mashindano ya Riadha Duniani mwaka ujao mjini Tokyo Japan.