Makabiliano baina ya kambi mbili hasimu za chama cha United Democratic Alliance, UDA yalisababisha kutibuka kwa mkutano wa wajumbe wa chama hicho katika tawi la Mombasa.
Wafuasi wa mbunge wa Nyali Mohamed Ali na wale wa mbunge wa bunge la Afrika mashariki Hassan Omar, walikabiliana katika mkutano uliohudhuriwa na katibu mkuu wa chama hicho Cleophas Malala na kuandaliwa katika chuo cha maongozi cha serikali mjini Mombasa.
Mkutano huo ulikuwa umeitishwa kuzindua mchakato wa kuwasajili wanachama wapya mjini humo.
Ghasia zilizuka baada ya Omar kuingia ukumbini huku umati ukijaribu kumzuia Ali kuingia katika eneo la mkutano.
Hii iliwalazimisha polisi kurusha vitoza machozi.
Akiwahutubia wanahabari, Malala alisema kuwa chama hicho kitachunguza swala hilo na kuwaita viongozi husika ili kubaini chanzo cha purukushani hiyo.