Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga ameelezea wasiwasi kuhusiana na ripoti za visa vinayoshukiwa kuwa utekaji nyara na kutoweka kwa Wakenya katika njia ya kutatanisha.
Katika taarifa aliyotoa jana, Ingonga aliangazia visa vitatu vya aina hiyo vya mwezi Disemba pekee vinavyohusisha wahasiriwa Bill Mwangi, Peter Muteti Njeru na Bernard Kavuli.
Watatu hao hawajulikani waliko baada ya kuchukuliwa kutoka sehemu mbalimbali na watu wasiojulikana katika mazingira ya kutatanisha.
Ingonga alisisitiza jukumu la serikali la kulinda haki ya kuishi na ulinzi wa kibinafsi ambazo zimekitwa kwenye katiba ya nchi.
Alitambua uchunguzi unaoendelea wa mamlaka huru ya kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA) na huduma ya taifa ya polisi kuhusu visa hivyo.
Kutokana na uzito wa madai hayo na wito kutoka kwa umma, Ingonga ameagiza asasi hizo mbili kuharakisha uchunguzi na kutoa taarifa kwa afisi yake katika muda wa siku tatu.
Aliahidi kwamba afisi yake itashughulikia kesi hizo kulingana na sheria ikitoa kipaumbele kwa haki na kuzuia matumizi mabaya ya michakato ya kisheria.