Mkewe Rais Rachel Ruto ameanzisha mpango wake wa kuandaa tamasha za muziki wa injili katika kaunti zote 47 kupitia kwa shirika lake la “MaMa Doing Good” na kaunti ya kwanza kunufaika ni Narok.
Tamasha hiyo iliandaliwa jana jioni katika uwanja wa michezo wa Ole Ntimama na ilihudhuriwa na wawakilishi wa shirika la hakimiliki ya muziki nchini, MCSK akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Ezekiel Mutua na Mkurugenzi wa MCSK eneo la Rift Valley Paul Maina.
Rachel alianzisha mpango huo wa tamasha za muziki kwa lengo la kurejesha maadili katika tasnia ya nyimbo za injili na kukita mizizi ya kitamaduni katika jamii kupitia nyimbo.
Dhamira nyingine ni kutambua na kukuza talanta za muziki mbali na kutoa jukwaa la kuonyesha talanta hizo.
MCSK inashirikiana na shirika la “Mama Doing Good” kwenye mipango yake ya kuwezesha jamii hasa mpango wa kuhuisha muziki wa injili ulio bora na kukuza talanta.
Mpango huo ulianzishwa katika ikulu ya Nairobi Julai 25, 2023 kwenye mkutano ambao mama taifa aliandaa na waanzilishi wa muziki wa injili nchini wapatao 36.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kufahamu matatizo yanayokumba sekta ya muziki na kutafuta njia za kuiimarisha kama nguzo muhimu katika uchumi.
Waliohudhuria mkutano wa siku hiyo ni wanamuziki Bwana na Bi. Kasanga, Esther Wahome, Munishi, Rose Jeffa, Peace Mulu na Hellen Mtawali kati ya wengine.