Mipango ya kumfurusha Gavana wa Nyamira yakamilika

Tom Mathinji
1 Min Read

Wawakilishi wadi kaunti ya Nyamira, wamekamilisha mswada wa kumfurusha Gavana wa kaunti hiyo Amos Nyaribo kwa madai ya utepetevu.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika kaunti hiyo Duke Masira, Wawakilishi hao wa wadi, walisema hawawezi vumilia kiwango cha juu cha ufisadi dhidi ya Gavana Nyaribo.

Gavana huyo analaumiwa kwa kutokamilisha miradi huku mingine ikikwama.

“Tumepokea malalamishi kutoka kwa wakazi wa kaunti hii wakisema tangu watuchague afisini, hawaoni miradi yoyote ya maendeleo, au kukamilishwa kwa miradi iliyokwama. Wanapanga kuandaa maandamano kwa sababu hatuwahudumii,” alisema Duke Masira.

Mwakilishi wadi ya Kiabonyoru Vincent Benecha, alithibitisha kuwa wamekusanya Saini  28 kati ya 34 na wameziwasilisha kwa karani wa bunge hilo ili atayarishe mswada wa kumfurusha Gavana huyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wadi mteule Abigael Matini, alisema hawatatishwa kwa kupewa hongo kwa kuwa ni mwananchi wa kawaida anayeumia.

Matini alisema watawasilisha mswada wa kumbandua Gavana huyo Jumanne tarehe 26 mwezi huu.

Share This Article