Serikali kuu, serikali za kaunti, shirika la msalaba mwekundu na mashirika mengine ya msaada yanatoa msaada wa dharura kwa jamii katika kaunti zilizoathiriwa na mafuriko.
Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani na usimamizi wa kitaifa ambayo ilitaja ripoti ya shirika la utabiri wa hali ya hewa, lililotabiri uwepo wa mvua kubwa mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu.
Katika taarifa wizara hiyo ilisema maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na eneo la ziwa Victoria Basin, Miinuko ya magharibi na mashariki mwa Rift Valley, katikati na kusini mwa Rift Valley zikiwemo kaunti za kaskazini magharibi kama Turkana na Samburu.
Eneo la Nairobi kaunti za Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu,
Laikipia mashariki, Meru, Embu, Tharaka Nithi.
Maeneo ya chini kaunti za eneo la kusini mashariki kama Kitui, Makueni, Machakos, Taita Taveta, na Kajiado.
Kaunti za kaskazini mashariki kama Mandera, Marsabit, Wajir, Garissa na Isiolo na kaunti za eneo la Pwani kama Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale.
Wizara hiyo inasema makundi ya kushughulikia majanga na yale ya ulinzi yametumwa katika maeneo husika na yanasaidia kutambua maeneo ambayo huenda yakazungukwa kabisa na maji ya mafuriko.
Wanatumia ndege pamoja na usafiri wa ardhini.
Imesema pia kwamba walinzi wa pwani, waafisa wa polisi, wanajeshi wa KDF na askari wa kutunza wanyamapori wako ange kuokoa watakaoathiriwa na mafuriko.
Makundi hayo yatagawa chakula na vifaa vingine kwa jamii zilizoathirika ambazo ziko katika maeneo zilikohamishiwa.
Jamii hizo zimepatiwa makazi ya muda katika mahema, majengo ya shule na kumbi za kijamii.
Jamii zinazoishi katika maeneo ambayo huenda yakaathirika na mafuriko zinashauriwa kuhamia maeneo salama, huku hali ya barabara na madaraja ikifuatiliwa.