Maafisa wa uokoaji wamepata mili yote mitatu ya wahasiriwa wa ajali ya mashua, iliyokuwa ikishiriki mashindano ya uendeshaji mashua, katika kijito cha Tudor, Bahari ya Hindi kaunti ya Mombasa.
Mkasa huo ulitokea wakati mashua iliyokuwa ikishiriki kwenye mashindano ikiwa imewabeba 22 ilipopinduka na kusababisha vifo vya watu watatu.
Maafisa wamesema kuwa miili hiyo iliopolewa wakati wa shughuli ya uokoaji iliyotekelezwa na mashirika mbalimbali yakiongozwa na jeshi la wanamaji la Kenya.
Kufuatia kisa hicho serikali ya kaunti ya Mombasa imetangaza hatua mpya za usalama baharini zinazonuiwa kuepusha ajali baharini katika nyakati za baadaye.
Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir amesema sasa wanaratibu viwango na sera bayana za kuongoza shughuli za baharini kwenye bahari ya Hindi.
Kadhalika aliagiza kutolewa kwa ushauri nasaha kwa manusura na familia zilizowapoteza wapendwa wao.
Uchunguzi kamili kuhusiana na kisa hicho utatekelezwa kwa pamoja na huduma ya ulinzi wa pwani humu nchini na maafisa wa idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai.
Wakati huo huo, Gavana huyo aliagiza hoteli na taasisi zote zilizo kwenye ufuo ni sharti sasa zipate idhini kutoka kwa makundi ya usalama na kushughulikia majanga katika kaunti hiyo kabla ya kuandaa hafla kubwa karibu na, au baharini.