Baraza la Sanaa la Taifa nchini Tanzania linaripoti kwamba naibu waziri wa utamaduni, sanaa na michezo, nchini humo Hamis Mwinjuma, alimzuru msanii mkongwe Zahir Ally Zorro maarufu kama Mzee Zorro.
Mbunge huyo wa eneo la Muheza maarufu kama Mwana FA alifika nyumbani kwa Zorro huko Kigamboni jijini Dar es salaam Novemba 9 2024, na kumpatia msaada wa vifaa vya mazoezi.
Hiyo ilikuwa sehemu ya ahadi yake kwa Mzee Zorro aliyotoa siku chache zilizopita akiwa kwenye uzinduzi wa vionjo vya album ya Fid Q na Lord Eyes iitwayo “Neno”.
Mzee Zorro alimshukuru Mungu sana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Hamis Mwinjuma kama naibu waziri na ambaye aliitikia kwa haraka suala lake.
“Mungu ambariki sana, Nitaendelea kumuombea. Mimi siumwi chochote, ni kwa sababu ya hii miaka sabini. Nitavitumia vifaa hivi, nitaanza kidogo kidogo kwa mikono, baadaye nitaanza kuitumia baiskeli, Naamini nitakaa sawa.” alisema Mzee Zorro.
Mheshimiwa Mwinjuma aliahidi kuendelea kumfuatilia Mzee Zoro kwa karibu hadi atakaporejelea hali yake ya kawaida, aidha alisema msaada huo unadhihirisha dhamira ya Serikali katika kutambua mchango wa wasanii wa sanaa zote na kuwasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika maisha yao.
Hatua ya Mwinjuma inajiri baada ya Mzee Zorro ambaye ni mwanamuziki kufika kwenye tamasha akitumia kiti cha magurudumu.
Zorro alianza kuimba kwenye bendi ya Super Vea ya huko Mwanza mwaka 1969 hadi 1973 kabla ya kujiunga na bendi ya Mara jazz.
Hakukaa huko sana akarejea nyumbani na Novemba 1, 1973 akaajiriwa kazi ya uanajeshi.
Aliimba katika bendi ya jeshi iliyofahamika kama Kimulimuli Orchestra hadi alipojiuzulu jeshini mwaka 1989.
Mwana uliofuata alijiunga na bendi ya Sambalumaa alikokaa hadi mwaka 1995 kisha akawa mwanamuziki wa kujitegemea.