Mamake mwanamuziki tajika Beyonce, Tina Knowles aliungana tena na aliyekuwa mume wake na baba ya watoto wake Mathew Knowles, anapoendelea kutangaza kitabu chake kiitwacho “Matriarch”.
Tina alikumbuka jinsi aliuliza Mathew awali iwapo angetaka kuungana naye katika eneo la Houston anapoendeleza ziara yake ya kukitangaza kitabu hicho.
Katika kikao cha kutangaza kitabu hicho huko Houston Jumatatu, Tina alikuwa pamoja na Kelly Rowland ambaye aliongoza mazungumzo hayo kabla ya wawili hao kumwalika jukwaani Mathew.
Tina aliambia umati uliokuwepo kwamba yeye na Mathew hawajawai kusemana vibaya na hawatawahi huku akimtaja mume huyo wake wa zamani kuwa mtu mwenye neema nyingi.
Wawili hao, Tina wa umri wa miaka 71 na Mathew wa miaka 73, walizungumzia jinsi waliwalea wanao Beyoncé na Solange huku wakiangazia kumbukumbu za uundaji wa kundi la muziki la Destiny’s Child.
Tina na Mathew walifunga ndoa mwaka 1980 kabla ya kubarikiwa na mabinti zao Beyoncé wa umri wa miaka 43 na Solange wa umri wa miaka 38.
Baada ya ndoa ya miongo mitatu, Tina alianzisha mchakato wa talaka mwaka 2009 kutokana na kile alichokitaja kuwa Mathew kutokuwa mwaminifu kwa ndoa yao na tayari alikuwa amepata mtoto na mwanamke mwingine.
Mwaka 2011 aliwasilisha ombi jingine la talaka, mchakato uliokamilishwa mwaka huo huo.
Baada ya kuzindua kitabu chake, Mathew alitumia mitandao ya kijamii kumpongeza mke wake wa zamani Tina. Kitabu hicho ‘Matriach’ kilizinduliwa rasmi Aprili 22, 2025 na kinasemekana kuwa na mauzo mazuri.