Mgomo wa wahadhiri: Serikali kukutana na maafisa wa UASU kuondoa utata

Martin Mwanje
2 Min Read
Julius Migosi - Waziri wa Elimu

Waziri wa Elimu Julius Migosi ametangaza kuwa serikali leo Jumatano alasiri itakutana na maafisa wa Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, UASU ili kutatua utata unaozingira utekelezaji wa makubaliano yao ya awali ya kurejea kazini. 

Kulingana na Migosi, utata huo unatokana na kiwango cha fedha wanazopaswa kulipwa wahadhiri hao kama ilivyokubaliwa kwenye makubaliano hayo yaliyosababisha kusitishwa kwa mgomo wa awali.

“Changamoto kati yetu na UASU juu ya makubaliano ya kurejea kazini ya wahadhiri ni kwamba tulikubaliana juu ya nyongeza ya mshahara ya asilimia 7 na 10 lakini takwimu ambayo serikali inayo na ile ambayo UASU inayo inatofautiana kwa karibu shilingi bilioni tano,” amesema Waziri alipofika mbele ya Bunge la Seneti leo Jumatano asubuhi.

Migosi amesema hii ndio sababu Wizara yake imeandaa mkutano na maafisa wa UASU leo alasiri ili kubaini kiini cha tatizo hilo na kisha kulitatua haraka iwezekanavyo.

Matamshi yake yanajiri wakati mgomo wa wahadhiri ambao umelamaza masomo katika vyuo vikuu vyote va umma kote nchini ukiingia siku ya pili leo Jumatano.

UASU, kupitia Katibu Mkuu wake Dkt. Constantine Wasongaimetangaza kwamba mgomo huo utaendelea hadi pale ambapo serikali itatimiza matakwa yao kama yalivyo kwenye makubaliano ya pamoja ya mwaka 2012 hadi 2025.

Dkt. Wasonga anaitaka serikali kutekeleza yaliyomo kwenye makubaliano ya kurejea kazini yalio na mafao mengi kwao.

Wahadhiri hao wameapa kutorejea kazini hadi walipwe pesa wanazodai huku wakishtumu manaibu chansela wa vyuo vyao kwa kuwa kizingiti kwa mipango yao ya kutafuta malipo bora.

Dkt. Wasonga amesisitiza hakuna mhadhiri ataonekana kwenye kumbi za masomo kutoa huduma kwa wanafunzi hadi matakwa yao yatimizwe.

Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, wahadhiri walisitisha mgomo baada ya kuafikia makubaliano na serikali kwamba wangeongezwa mshahara kwa asilimia 10.

Walikuwa wametoa ilani ya siku saba ya kugoma iliyokamilika Jumatatu usiku wa manane.

Share This Article