Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi amehudhuria mkutano wa pamoja wa mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuangazia hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkutano huo umefanyika leo Jumatatu mjini Harare nchini Zimbabwe.
Mudavadi alikuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo pamoja Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Prof. Amon Murwira.
Prof. Murwira pia ni mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC.
Mkutano huo unakuja kfuatia maazimio ya Dar es Salaam ya mkutano wa pamoja wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Februari 8, 2025.
Mkutano wa leo Jumatatu mjini Harare ulitarajiwa kuratibu mpango madhubuti wa kutafuta amani unaoangazia kiini cha mgogoro unaoshuhudiwa kwa sasa mashariki mwa DRC.
Mkutano huo, kadhalika, ulitarajiwa kuangazia namna ya kubadili hali ya kisiasa ndani ya DRC.
Awali, Mudavadi aliongoza mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa EAC juu ya hali ya usalama nchini DRC.
Aliandamana na Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya.
Waasi wa M23 wamechukua udhiti wa mji wa Goma mashariki mwa DRC na wametangaza pia kuchukua udhibiti wa mji wa Bukavu katika hatua ambayo imesababisha kuzorota kwa hali ya usalama nchini DRC.
Angola inaongoza juhudi za kuzipatanisha pande zinazozozana.