Mfanyakazi wa Microsoft avuruga hafla ya kampuni kulalamikia uhusiano na Israel

Mwanamke huyo kwa jina Ibtehal Abu Saad, alilalama kuhusu hatua ya Microsoft ya kuuzia jeshi la Israel programu za akili unde.

Marion Bosire
1 Min Read

Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya Microsoft alivuruga hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya uwepo wa kampuni hiyo Ijumaa kulalamikia uhusiano wake na Israel.

Mwanamke huyo kwa jina Ibtehal Abu Saad, mzaliwa wa Morocco aliyesomea katika chuo kikuu cha Havard alilalama kuhusu hatua ya Microsoft ya kuuzia jeshi la Israel programu za akili unde.

Ibtehal aliingia jukwaani katika ukumbi wa hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya kampuni hiyo ya Microsoft ambayo ilihudhuriwa na mmiliki Bill Gates na akamtaka afisa mkuu mtendaji wa tawi la akili unde kukomesha hatua za kuwezesha mauaji ya halaiki Gaza kupitia huduma za Azure, seva na mikataba ya teknolojia na jeshi.

“Hatuwezi kuwa tunasherehekea huku watu wakiuawa Palestina kutokanana usaidizi wa kampuni ya Microsoft” Ibtehal aliambia wanahabari.

Alizungumza na wanahabari baada ya kuondolewa kwenye ukumbi wa hafla hiyo ambapo alisema anajua huenda akachukuliwa hatua lakini woga alionao ni kwamba kazi zao zinachangia katika mashambulizi ya mabomu, ufuatiliaji na kulengwa kwa watu wasio na hatia.

“Wanaweza wakaniandama kufuatia nilichosema lakini woga wangu ni kuamka siku moja na kufahamu kwamba alama ya siri niliyounda imehusika katika mauaji ya watoto” alimalizia kusema Ibtehal.

Website |  + posts
Share This Article