Mfalme Charles III wa Uingereza na Malkia Camilla wameondoka nchini leo Ijumaa baada ya kukamilisha ziara yao ya siku nne.
Hiyo ilikuwa ziara rasmi ya kwanza ya Mfalme Charles III na Malkia Camilla katika taifa la Afrika na ya kwanza katika taifa la Jumuiya ya Madola tangu aliposhika hatamu za uongozi mwezi Mei mwaka 2023.
Rais William Ruto aliwaaga wawili hao katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Moi jijini Mombasa.
Mfalme Charles III na Malkia Camilla waliwasili nchini Jumatatu wiki hii wakiwa wameabiri ndege ya jeshi la wanahewa la Uingereza muda mfupi kabla ya saa tano asubuhi.
Wakati wa dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais William Ruto, Mfalme Charles alielezea majuto na huzuni mkubwa kutokana na dhuluma zilizotekelezwa na serikali ya Uingereza dhidi ya Wakenya wakati wa harakati za kupigania uhuru wa taifa hili.
Mfalme huyo alisema hayo wakati wa dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Rais William Ruto na Mama Rachel Ruto Jumanne jioni katika ikulu ya Nairobi.
Alikariri umuhimu wa pande zote mbili kushughulikia dhuluma hizo za kihistoria kwa njia iliyo wazi.
“Ni muhimu sana kwangu kukutana na baadhi ya wale maisha yao na jamii zao ziliathiriwa pakubwa na dhuluma hizo,” alisema Mfalme Charles.
Wakati wa ziara yake nchini, Mfalme Charles na Mkewe walizuru maeneo mbalimbali katika kaunti za Nairobi na Mombasa.
Akiwa Mombasa alikofanya ziara ya siku mbili, Mfalme Charles alizuru eneo la wanajeshi wa majini la Mtongwe Naval Base katika kaunti ya Mombasa.
Akiwa huko, alishuhudia onyesho la kipekee la kutua ufuoni lililoandaliwa na wanajeshi wa majini wa Kenya na Uingereza chini ya wakufunzi wao wa British Royal Marines.