Meli ya pili ya kifahari yatia nanga Mombasa

Tom Mathinji
2 Min Read
Meli ya watalii yatia nanga Mombasa.

Kulikuwa na furaha isiyo kifani katika bandari ya Mombasa, baada ya meli nyingine ya kifahari kwa jina MV  World Odyssey, kutia nanga ikiwa na wageni 763.

Meli hiyo iliwasili katika bandari hiyo Ijumaa asubuhi ikiwa na wanafunzi 585, wakufunzi 178 na wafanyakazi 198.

Kuwasili kwa meli hiyo ya kifahari na ambayo ni ya pili kuwasili hapa nchini mwaka huu, kunaashiria kuimarika kwa sekta ya utalii wa meli hapa nchini.

Meli hiyo ya MV World Odyssey iliyotengenezewa nchini Ujerumani mwaka 1998, hutumika kama taasisi ya elimu na inatarajiwa kuwa katika bandari ya Mombasa kwa siku sita.

Wanafunzi walio katika meli hiyo wametoka mataifa 20 na wakemuwa katika meli hiyo kwa kati ya siku 100 na 105.

Aidha wanafunzi hao watabadilishana mawzo na wenzao kutoka chuo cha kiufundi cha Mombasa na chuo kikuu cha Kenyatta bewa la Mombasa.

“Tumefurahi kupokea meli hii, tunatarajia meli zaidi mapema mwezi Machi, ili tuwe na watalii wengi wanaowasili kwa meli na hivyo kuimarisha uchumi wetu,” alisema afisa mkuu wa halmashauri ya bandari nchini nahodha Capt. Ali Abdille.

Kwa upande wake mkuu wa uhusiano mwema na mawasiliano katika bodi ya utalii nchini Wausi Walya, alisema kuwasili kwa meli hiyo ni hakikisho bandari ya Mombasa ni ya kupigiwa mfano.

Walya alidokeza kuwa Meli hiyo itapiga jeki uchumi wa taifa hili, huku watalii hao wakizuru maeneo tofauti ya eneo hilo.

Kulingana na Walya utalii wa Meli umeimarika kwa asilimia 50 mwaka huu.

Tangu mwezi Januari mwaka huu meli mbili za kifahari zimetia nanga katika bandari ya Mombasa, zikiwa na zaidi ya watalii 6,000.

Mwaka uliopita, watalii 3,123, waliwasili hapa nchini kupitia meli za kifahari.

Share This Article