Mchekeshaji Fred Omondi ambaye ni kakake msanii maarufu Eric Omondi, amefariki baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani.
Kulingana na taarifa ya polisi, Fred Omondi alikuwa amebebwa kwenye pikipiki wakati ilipogongana ana kwa ana na basi moja la abiria kwenye barabara ya Kangundo Jumamosi asubuhi.
Polisi wanasema dereva wa pikipiki hiyo pia alipata majeraha mabaya mguuni, na anapokea matibabu katika hospitali ya Mama Lucy.
“Ajali hiyo ilihusisha basi aina la Mistubishi yenye nambari za usajili KCC 126A ambalo liligongana ana kwa ana na pikipiki iliyokuwa ikitoka upande wa pili. Katika ajali hiyo Fred Odhiambo Omondi alifariki papo hapo,” ilisema taarifa ya polisi.
Kupitia mtandao wake wa Instagram, mchekeshaji Erick Omondi alielezea kuhuzunishwa na kifo cha kaka yake akisema, “Safiri salama ndugu yangu”.
Kupitia mitandao ya kijamii, Wakenya wamemuomboleza Fred, huku wakituma jumbe za faraja kwa familia yake.