MCAs Isiolo wafanya kikao cha kwanza tangu jaribo la kumbandua Gavana Guyo

Martin Mwanje
3 Min Read

Wawakilishi Wadi wa Bunge la Kaunti ya Isiolo (MCAs) jana Jumanne walifanya kikao chao cha kwanza tangu jaribio la kutaka kumbandua madarakani Gavana Abdi Ibrahim Guyo. 

Hoja ya kumbandua Guyo ilitupiliwa mbali na Seneti katika hatua za awali kwa misingi ya dosari za kisheria, baada ya Bunge la Kaunti kushindwa kuthibitisha kuwa kulikuwa na kikao halali cha kuwasilisha hoja hiyo na hatimaye kumbandua.

Mamia ya wakazi wa Isiolo waliounga mkono jaribio hilo walifurika mjini Isiolo kuwapokea Wawakilishi hao waliokuwa wamekimbia eneo hilo wakihofia usalama wao tangu walipoanza mchakato wa hoja ya kumtimua  Gavana huyo.

Katika kikao hicho, Spika Mohamed Roba Qoto alitangaza kuwa ofisi yake ilikuwa imepokea barua rasmi kutoka kwa Chama cha United Democratic Movement (UDM), ikieleza kuwa wanachama wao wawili walioteuliwa kuiwakilisha UDM katika Bunge la Kaunti ya Isiolo — Fozia Djibril Bore na Amina Omar Enow — walikuwa wamefutwa kutoka orodha ya wanachama wa chama hicho, na hivyo basi hawatakuwa tena wajumbe wa bunge hilo kwa sababu hawawezi kuendelea kuiwakilisha UDM wakiwa si wanachama.

Spika Roba alitaja madai ya utovu wa nidhamu na kushindwa kuchangia fedha za kila mwezi kwa chama kama baadhi ya sababu zilizotolewa na UDM kwa kuwachukulia hatua wawakilishi hao wawili.

Wawili hao walikuwa miongoni mwa MCAs 16 waliounga mkono hoja ya kumwondoa Gavana Guyo, lakini walihamia upande wa Gavana siku nne zilizopita, hali iliyompa afueni ya muda Guyo baada ya hoja hiyo kushindwa kupenya Seneti.

Aidha, Spika Roba alitoa taarifa kuwa MCA wa Wadi ya Oldonyiro ambaye pia ni Naibu Spika, David Lemantile (KANU), alikuwa ameondolewa kutoka Kamati ya Sheria, Kanuni na Haki za Bunge na nafasi yake kuchukuliwa na MCA wa Wabera, Salesio Kiambi.

Francisco Letimalo (KANU) pia alipokonywa wadhifa wa Kiongozi wa Wachache Bungeni na nafasi hiyo ikachukuliwa na MCA wa Cherab, Halima Golle Abgudo, naye pia akiwa wa chama cha KANU.

Wawakilishi Wadi hao wanne waliopokonywa nyadhifa ni sehemu ya kundi la watano (pamoja na MCA mteule Rahma Abdkadir – KANU) waliojiunga na kambi ya Gavana Guyo siku chache zilizopita, kufuatia kushindwa kwa hoja ya kumwondoa Gavana kupita Seneti.

Wakihutubia umma uliokuwa umejitokeza kuwapokea mjini Isiolo, Wawakilishi Wadi hao walitoa hakikisho kwa wakazi wa Isiolo kwamba wamepania upya kuisimamia serikali ya kaunti kikamilifu na kuikosoa inapofeli, huku wakionya kuwa wako tayari kufufua tena hoja ya kumng’oa Gavana Guyo iwapo hatashughulikia changamoto zilizopo na kuimarisha utoaji huduma kwa wakazi wa Isiolo.

Walisema pia kuwa watasimama imara kumuunga mkono Spika wao.

Share This Article