Mbosso aondoka WCB

Baba Levo ndiye alitangaza hayo akisema kwamba nidhamu ya Mbosso na heshima yake vimempendelea na hivyo hatalipa chochote.

Marion Bosire
2 Min Read
Mbosso Khan, Mwanamuziki Tanzania

Msanii wa muziki nchini Tanzania Mbwana Yusuf Kilungi maarufu kama Mbosso anaripotiwa kuondoka kwenye kampuni ambayo imekuwa ikimsimamia ya Wasafi Classic Baby – WCB.

Mtangazaji maarufu wa redio nchini Tanzania Baba Levo ndiye alitangaza hayo kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo alisema kwamba nidhamu ya Mbosso na heshima yake vimempendelea.

Kulingana na Baba Levo, Mbosso ataruhusiwa kuondoka bila kulipa chochote kwa kampuni ya WCB kinyume na ilivyokuwa kwa Harmonize alipoondoka.

Ripoti nyingine zinaashiria kwamba wasimamizi wa kampuni hiyo ya WCB wamekatiza mkataba wa Mbosso aondoke ili aache nafasi kwa wasanii wapya tisa ambao huenda wakasajiliwa mwaka huu wa 2025.

“Nidhamu Kubwa Ya Mbosso imemfanya Diamond Platnumz amsamehe mamilioni ya pesa na Kumpa Uhuru wa kwenda kupambana nje ya WCB! Hii inawapa nafasi WCB kusaini wasanii wengine wapya mwaka huu wa 2025.” ndiyo maneno aliyoandika Baba Levo.

Mbosso Khan aliyezaliwa Oktoba 3, 1995 alisajiliwa kwenye WCB mwaka 2017 baada ya mapumziko ya mwaka mmoja kutoka kwa tasnia ya muziki.

Kabla ya hapo alikuwa mmoja wa wanachama wa kundi la muziki la Yamoto Band iliyokuwepo kati ya mwaka 2013 na 2015 na akiwa humo alikuwa anajiita ‘Maromboso’.

Katika WCB ndipo alipata fursa ya kufanya kazi kama mwanamuziki wa peke yake na alitoa nyimbo kama ‘Maajabu’, ‘Picha Yake’, ‘Tamu’ na ‘Tamba’.

Tangu wakati huo amekua kwa kiwango kikubwa kama mwanamuziki huku akionyesha weledi wake.

Alizindua EP yake ya kwanza iitwayo ‘Khan’ Novemba 2022. Ilihusisha nyimbo za mapenzi na ni mojawapo ya EP ambazo zilisikilizwa sana kwenye jukwaa la Boomplay nchini Tanzania ambapo ilisikilizwa zaidi ya mara milioni 50.

Mwaka 2023 Mbosso alikuwa mmoja wa wasanii wachache wa Tanzania waliotimiza kiwango kikumbwa cha usikilizaji wa nyimbo zake kwenye Boomplay ambapo nyimbo zake zilisikilizwa zaidi ya mara milioni 200.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *