Mtu mmoja alifikishwa katika mahakama ya Milimani kuhusiana na kupatikana kwa magunia 252 ya mbolea ya serikali iliyoibwa na kushtakiwa kwa kusafirisha mali ya wizi.
Idara ya upelelezi wa jinai, DCI inasema mbolea hiyo ilipatikana ikiwa imehifadhiwa katika ukumbi wa kanisa la Grace Covenant mjini Narok jana Jumatano.
Robert Kipng’etich Bett almaarufu Raphael aliyedai kuwa msimamizi wa shamba aliyeajiriwa na mfanyabiashara Joseph Kiplangat Keter kutoka Kericho alikamatwa katika eneo la Ololulunga, Narok Kusini.
Alisemekana kuwa mmiliki wa mbolea iliyopatikana ikiwa imehifadhiwa katika ukumbi wa kanisa la Grace Covenant.
Mshukiwa wa pili alidai kununua mbolea hiyo ya serikali kutoka kwa muuzaj anayejulikana na anayeendesha shughuli zake katika eneo la North Rift.
Wakati uchunguzi ukiendelea, mshukiwa aliyefikishwa mahakamani aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi nusu milioni pesa taslimu.
DCI inasema kikao cha kwanza cha kusikilizwa kwa kesi hiyo kitafanyika kesho Ijumaa, Januari 5, 2024.