Wafanyakazi wa kampuni ya biashara ya kimataifa ya Africalink wapo kwenye pirikapirika za kupakia mizigo kwenye kontena tunapowasili kwenye ghala yao.
Ghala hiyo inapatikana katika bandari ya nchi kavu ya Yiwu katika mkoa wa Zhejiang, kusini mashariki mwa China.
Lengo la wafanyakazi hao ni kupakia mizigo hadi kuijaza kontena inayolenga kusafirishwa hadi nchini Burundi kufikia wakati jua likizama siku hiyo.
Mizigo inajumuisha bidhaa kama vile nguo, vitambaa, tarakilishi na vifaa tiba.
“Kampuni yetu inasafirisha mizigo katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Burundi, Tanzania, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC na Rwanda,” anasema afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo ambaye hakutaka kutajwa kwa jina.
“Hata hivyo, tumesitisha usafirishaji mizigo kwenda DRC kwa sababu ya mgogoro unaoshuhudiwa mjini Goma,” anaongeza afisa huyo wakati shughuli za upakiaji mzigo zikipamba moto kwenye ghala hiyo.
Nazo pirikapirika za upakiaji mizigo kwenye ghala hiyo zinaakisi shughuli nyingi za upakiaji mizigo zinazoendelea katika maeneo mbalimbali ya bandari hiyo ya nchi kavu ya Yiwu.
Sawia na Soko la Biashara ya Kimataifa la Yiwu, Bandari ya Nchi Kavu ya Yiwu pia imegawanywa katika maeneo maalum ambayo hujishughulisha na usafirishaji wa mizigo mahususi.
Kwa mbali, utaona rundo la makontena yanayosubiri kupakiwa mizigo kuelekea bandari za bahari ikiwemo ile ya Ningbo-Zhoushan.
Punde shughuli ya upakiaji kwenye kontena ikimalizika, kontena hizo hunyanyuliwa kwa mashine maalum na kuwekwa kwenye treni na kisha kusafirishwa hadi bandari za bahari.
Kisha mizigo hiyo husafirishwa kupitia Bahari ya China Mashariki hadi nchi za Afrika na barani Ulaya.
Mbali na usafirishaji wa mizigo kupitia bahari, kunayo pia treni ya moja kwa moja inayotumiwa kusafirisha mizigo kati ya China na Ulaya, maarufu kama “China-Europe Express.
Bidhaa zinazosafirishwa kupitia kwenye treni hiyo ni pamoja na magari, bidhaa za ujenzi, samani na mashine.
Mifumo hiyo ya usafirishaji, bila shaka, imekuwa nguzo muhimu katika kuboresha biashara kati ya China, Afrika na bara la Ulaya.