Rais William Ruto amewaelezea Wakenya kwamba serikali itahakikisha mbolea ya bei nafuu inapatikana kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa upanzi.
Amefutilia mbali hofu ya kuwepo janga katika sekta ya kilimo kutokana na mahitaji ya juu ya mbolea ya bei nafuu kabla ya kuanza kwa msimu wa upanzi baadaye mwezi huu.
Akizungumza wakati akizindua Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji katika kaunti ya Kakamega linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Rais alisema kila kitu kinafanywa kuhakikisha mbolea hiyo inapatikana kabla ya msimu ujao wa upanzi.
“Nataka kuwahakikishia wakulima kwamba serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha mbolea ya bei nafuu inapatikana,” alisema Ruto.
Wakati huohuo, kiongozi wa nchi alisema wale wanaouza mbegu na mbolea ya kiwango cha chini watakabiliwa na mashtaka ya uhalifu.
Amesema uchunguzi umeanzishwa kwa lengo la kuwakamata wale wanaouza mbegu na mbolea bandia.
“Hii leo tu, tumewakamata baadhi ya walaghai wanaotaka kutumia mpango wetu wa usambazaji wa mbolea ya bei nafuu na tunao wengine zaidi ambao wameshtakiwa mahakamani,” alisema Rais Ruto.
“Lazima tukabiliane na wale wanaotaka kuhujumu mpango wetu wa mbolea ya bei nafuu.”