Kamati ya bunge kuhusu uteuzi inatarajiwa kuwasaili mawaziri watatu wateule leo Jumanne alasiri katika ukumbi wa kaunti.
Watatu hao wanajumuisha Mutahi Kagwe aliyeteuliwa kuwa waziri wa kilimo na ustawi wa mifugo, Lee Kinyanjui (Biashara, viwanda na vyama vya ushirika) na William Kabogo (Habari na uchumi wa dijitali).
Kagwe ambaye ni waziri wa zamani wa afya, ndiye atakuwa wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula saa sita adhuhuri.
Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu William Kabogo, naye anatarajiwa kufika mbele ya kamati hiyo saa tisa alasiri, huku Gavana wa zamani wa Nakuru Lee Kinyanjui akitarajiwa kusailiwa saa kumi na moja jioni.
Iwapo watatu hao wataidhinishwa na bunge, Mutahi Kagwe atachukua mahala pa Dkt. Andrew Karanja ambaye aliteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Brazil, William Kabogo atachukua nafasi iliyokuwa ya Margaret Nyambura Ndung’u aliyeteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Ghana, huku Lee Kinyanjui akichukuwa wadhifa ulioshikiliwa na Salim Mvurya ambaye alihamishwa wizara ya michezo.