Mchakato wa kusaili mawaziri 21 wateule ili kubaini ufaafu wao katika kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri unaanza leo Alhamisi.
Mchakato huo utaendeshwa kwa siku nne na utamalizika Agosti 4, 2024.
Mawaziri wanne wateule wamepangiwa kupigiwa msasa na Kamati ya Bunge la Taifa inayoshughulikia Masuala ya Usaili.
Waziri mteule wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki atakuwa wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo kuanzia saa mbili asubuhi akifuatwa na Debra Mlongo aliyeteuliwa kumrithi Susan Nakhumicha katika Wizara ya Afya.
Prof. Kindiki anatarajiwa kukabiliwa na wakati mgumu hasa kuhusiana na mienendo ya polisi wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z.
Maafisa wa polisi walilaumiwa kwa ukatili uliodaiwa kusababisha makumi ya vifo vya waandamanaji huku wengine wakiuguza majeraha ya risasi.
Mawaziri wengine wateule waliopangiwa kufika mbele ya kamati hiyo leo Jumanne ni Alice Wahome (Ardhi), Migos Ogamba (Elimu) na Soipan Tuya (Ulinzi).
Kamati hiyo imeahidi kuendesha zoezi hilo la usaili kwa uwazi na bila upendeleo huku ikiahidi kuhakikisha ni mawaziri wateule wanaostahiki pekee watakaoruhusiwa kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri.
Lengo ni kumsaidia Rais William Ruto kutimiza ajenda ya serikali ya Kenya Kwanza kwa taifa hili.