Jumla ya Mawaziri sita waliohudumu katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa na Rais William Ruto wiki iliyopita wametajwa katika nusu ya kwanza ya Baraza Jipya la Mawaziri lililozinduliwa leo Ijumaa.
Akitangaza nusu ya Baraza jipya la Mawaziri, Rais Ruto amemdumisha Prof. Kithure Kindiki kuwa Waziri wa Usalama wa Kitaifa.
Aden Duale ataendelea kuhudumu kama Waziri wa Ulinzi.
Kwa upande mwingine, Alice Wahome ataendelea kuhudumu kama Waziri wa Ardhi huku Soipan Tuya akisalia kuwa Waziri wa Mazingira.
Davis Chirchir amedumishwa katika Baraza jipya ila amehamishiwa Wizara ya Barabara na Uchukuzi ambayo awali ilishikiliwa na Kpchumba Murkomen. Awali, Chirchir aliongoza Wizara ya Nishati ambayo wadhifa wake bado haujajazwa.
Waziri wa zamani wa Biashara Rebecca Miano ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.
Hata hivyo, uteuzi wao lazima uidhinishwe na bunge kabla ya mawaziri hao wapya kuteuliwa rasmi na Rais Ruto kuhudumu katika nyadhifa hizo.