Wanafunzi 14 ni miongoni mwa watu ambao wamethibitishwa kufariki kutokana na mapromoko ya ardhi yaliyotokea Jumamosi iliyopita katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Huku athari za mafuriko hayo zikidhihirika, serikali imeimarisha jitihada za kuhakikisha watahiniwa katika maeneo yaliyoathiriwa wanafanya mitihani ya kitaifa inayoendelea kwa sasa bila usumbufu.
Katibu katika Wizara ya Elimu Julius Bitok amesema watahiniwa katika shule za msingi na sekondari walioathiriwa moja kwa moja na maporomoko hayo wataweza kufanya mitihani yao ya Gredi ya 8, KJSEA na ya kidato cha nne, KCSE kama ilivyopangwa.
Bitok amesema helikopta, magari yanayoweza kusafiri eneo lolote na usafirishaji mwingine umewekwa kuhakikisha usambazaji na ukusanyaji wa karatasi za mitihani katika maeneo yaliyoathirika.
“Kama serikali, tumekusanya rasilimali zote kuhakikisha watahiniwa walioathiriwa wanaweza kuendelea na mitihani yao bila kutatizika. Tumefanya mipango ya kutosha kuhakikisha hakuna mtahiniwa hata mmoja atakosa kufanya mtihani kwa sababu ya hali ya hewa au janga la hivi karibuni,” alihakikisha Katibu Bitok.
Alisema Wizara ya Elimu inafanya kazi kwa karibu na ile ya Usalama wa Taifa, asasi zingine za serikali na serikali za kaunti kuzihamisha familia zilizoathiriwa ikiwa ni pamoja na watahiniwa na kuhakikisha wanapata vituo mbadala vya kufanyia mitihani.
Angalau madaraja matatu yaliharibiwa na maporomoko hayo na hivyo kuzuia usambazaji wa kotena za mitihani kwa shule.
Kwa mujibu wa katibu huyo, mvua kubwa zinazonyesha eneo hilo zimeathiri ama moja kwa moja au hali isiyokuwa ya moja kwa moja watahiniwa 1,867 wa shule za sekondari ya chini na juu.
Aliyasema hayo leo Jumatatu katika ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti katika eneo la Westlands jijini Nairobi aliposhuhudia klufunguliwa kwa kontena za mtihani wa kuandika wa KCSE ulioanza hii leo.
